Sunday 9 October 2016

WAWEKEZAJI WILAYANI SERENGETI WAHIMIZWA KUCHANGIA SHUGHULI ZA MAENDELEO

Habari toka Kitengo cha Habari na Mawasiliano HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI.




Serikali wilayani Serengeti imewataka wawekezaji kulipa kodi na kuchangia katika shughuli za maendeleo ndani ya Wilaya ya Serengeti.
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu (aliyesimama) akiongea na wadauwa maendeleo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.



Hayo yamejiri jana Oktoba 8 2016 katika katika kikao cha wadau wa maendeleo kilichoitishwa na Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Nurdin Babu alipokuwa akizungumza na wawekezaji waliopo wilayani Serengeti katika ukumbi wa mikutano wa Halmshauri.“Tunataka kukamilisha ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya na nyinyi ni wadau wetu wakubwa katika maendeleo” alisema Mheshimiwa Babu. Aidha Mheshimiwa Babu amesikitishwa na kitendo cha wawekezaji waliopo katika wilaya ya Serengeti kutochangia katika shughuli za maendeleo hali kadhalika kutojitokeza kabisa kwa wahusika wakuu wa makampuni pindi wanapohitajika.
Aidha Mwenyekiti wa Halamshauri ya Wilaya ya Serengeti Mheshimiwa Juma Porini Keya amezitaka kampuni zenye kambi za utalii wilayani Serengeti kulipa kodi na tozo stahiki kwa serikali ili kuiwezesha Serikali kupitia Halmashauri kutoa huduma bora kwa wakazi wa Serengeti. Katika hatua nyingine Mheshimiwa Porini ameziomba kampuni zenye kambi za utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuajili watu kutoka wilayani Serengeti “Naamini Serengeti wapo vijana wenye sifa za kuajiliwa katika kampuni za utalii hifadhini” alisema Mheshimiwa Porini.



Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini alimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa juhudi anazofanya kuhakikisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya unakamilika na kushauri iundwe kamati itakayo wajumuisha wahifadhi pamoja na kampuni za utalii kushughulikia suala la ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti.
Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ilianzisha mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya mjini Mugumu kuanzia mwaka wa bajeti 2007/2008 ili kuimarisha huduma kwa wagonjwa wanaopewa rufaa kutoka vituo 54 vya huduma ya afya vilivyopo wilayani na wale wanaotoka katika mji wa Mugumu na vijiji jirani. Aidha wazo la kujenga Hospitali hiyo liliungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kuona umuhimu wa ujenzi wa Hospitali hii ili kutoa huduma kwa jamii na wageni wajao nchini kutembelea vivutio vya Kitalii vilivyoko jirani na Mji wa Mugumu hasa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Mpaka sasa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya umekwama kutokana na Halmashauri kutopata fedha kukamilisha ujenzi wa Hospitali.








   Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Dk. Manyatta akifafanua jambo kwa wajumbe wa kikao.
Wajumbe wa Kikao walitembelea majengo ya Hospitali ambayo ujenzi umesimama, kutoka kushoto ni Dk Manyata (Mganga Mkuu wa Wilaya) katikati ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhe Juma Porini Keya, Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu.

 






No comments:

Post a Comment