Wednesday 5 October 2016

KATIBU TAWALA MKOA WA MARA AFANYA ZIARA WILAYANI SERENGETI

Habari toka Kitengo cha Habari na Mawasiliano- HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI


Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bw. Ado Stephen Mapunda, leo tarehe 5 Oktoba 2016 amefanya ziara ya kujitambulisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na kufanya mazungumzo na watumishi wa Halmashauri.
            Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Bw. Ado Stephen Mapunda akizungumza na watumishi wa
                                                           Halmashauri ya wilaya ya Serengeti.
Katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. Juma Hamsini alimpongeza  Bw. Mapunda kwa kuteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na kuahidi kufanya nae kazi kwa umoja ili kuleta maendeleo katika Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara kwa ujumla.

Mapunda alipata wasaa wa kuongea na watumishi ambapo aliwataka kufanya kazi kwa bidii licha ya kuzungukwa na mazingira magumu ya kazi pia kuwa wabunifu kwa kubuni miradi itakayowanufaisha wananchi wa Serengeti. Katibu Tawala amewataka watumishi wa umma kujiendeleza kielimu na kuongeza maarifa ili kuongeza ufanisi wa kazi wakiwa kazini “Msibweteke na elimu mlizonazo na kusahau kwenda kujiendeleza kielimu” alisema Mapunda. Aidha Mapunda amewataka watumishi wa umma kutumia vizuri kipato wanachopata kwa kujiwekea akiba na kufanya shughuli za maendeleo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhe. Juma Porini Keya ambaye pia alihudhuria kikao hicho amempongeza Bw. Mapunda kwa uteuzi na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Serengeti na kuwataka watumishi wa Halmashauri kuyafanyia kazi yale yote aliyosema Katibu Tawala Mkoa wa Mara.

Tarehe 10 Septemba 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli alimteua Bw. Ado Stephen Mapunda kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mara na kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Benedict Ole Kuyan ambaye amestaafu.

      Katibu Tawala Mkoa wa Mara (kushoto) Bw. Ado Stephen Mapunda Akiwasili katika
        Ukumbi wa Mikutano wa Halamshauri, kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti
 Bw. Cosmas Qamara

     Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri yaWilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini (aliyesmama)
        akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa wa Mara tayari kwa mazungumzo na watumishi.

             Sehemu ya watumishi waliojitokeza kumsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Mara

No comments:

Post a Comment