Habari toka Kitengo cha TEHAMA & MAHUSIANO
HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI.
Mfuko
wa Singita Grumeti umeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuboresha hali ya
elimu katika Wilaya za Serengeti na Bunda.
Hii
imedhihirika kwenye halfa ya kukabidhi madawati 500 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara
Dk. Charles Mlingwa ili kupunguza uhaba wa madawati katika Wilaya hizo. Aidha
Grumeti wamekabidhi nyumba ya kuishi mwalimu iliyojengwa katika Shule ya Msingi
Makundusi.
“Tuko
hapa kukabidhi madawati haya 500 yenye thamani ya Tshs. Milioni 112 kwa Wilaya za
Serengeti na Bunda pamoja na nyumba hii yenye thamani ya Tshs. Milioni 86” alisema Richard Ndaskoi ambae ni Mkuu wa
Huduma za Jamii toka Mfuko wa Singinta Grumeti.
Akipokea
misaada hiyo, Dk. Mlingwa alisema “Nawashukuru Singita Grumeti kwa Msaada huu
wa madawati pamoja na nyumba hakika mchango wenu katika Mkoa wa Mara unaoneka”
Dk Mlingwa amewataka wawekezaji wengine katika Mkoa wa Mara kuchangia madawati
katika Wilaya za Serengeti na Bunda kwani bado zina uhaba wa madawati.
Aidha
Dk. Mlingwa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuwa na
mahusiano mazuri na wawekezaji waliopo katika Wilaya hiyo “Tukiwawekea
mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao hata wananchi pia watanufaika na uwepo
wa wawekezaji hawa” alisema Dk. Mlingwa.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bunda,
Lydia Bupilipili wote kwa nyakati tofauti wameushukuru Mfuko wa Singita Grumeti
kwa msaada huo wa madawati na kuuomba mfuko huo kuendelea kuchangia katika
shughuli za maendeleo katika Wilaya za Serengeti na Bunda. “Wilaya hii ina
wawekezaji wengi lakini wamekuwa nyuma katika kuchangia shughuli za maendeleo,
nawapongeza kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii inayowazunguka pamoja na
kuchangia katika maendeleo ya Wilaya ya Serengeti” alisema Nurdin Babu.
Aidha
Bi. Bupilipili ameuomba Mfuko huo kuanzisha kampeni maalumu ya kuongeza kiwango
cha ufaulu kwa watoto wa kike kwa shule za sekondari Wilayani Bunda.
Singita Grumeti wamekuwa wawekezaji wenye tija kwa
wananchi wa Wilaya za Serengeti na Bunda licha ya kuwa mstari wa mbele
kuchangia katika shughuli za maendeleo, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa ajira
kwa wakazi toka wilaya hizo mbili pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa
wanafunzi toka wilaya hizo.
No comments:
Post a Comment