Habari toka Kitengo cha Habari na Mawasiliano- HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI
Halmashauri ya wilaya ya Serengeti.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri yaWilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini (aliyesmama)
akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa wa Mara tayari kwa mazungumzo na watumishi.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara Bw. Ado Stephen Mapunda, leo tarehe 5 Oktoba
2016 amefanya ziara ya kujitambulisha katika Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti
na kufanya mazungumzo na watumishi wa Halmashauri.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Bw. Ado Stephen Mapunda akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Serengeti.
Katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. Juma Hamsini alimpongeza Bw. Mapunda kwa kuteuliwa na Rais John Pombe
Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara na kuahidi kufanya nae kazi kwa
umoja ili kuleta maendeleo katika Wilaya ya Serengeti na Mkoa wa Mara kwa
ujumla.
Mapunda alipata wasaa wa kuongea na watumishi ambapo aliwataka kufanya
kazi kwa bidii licha ya kuzungukwa na mazingira magumu ya kazi pia kuwa
wabunifu kwa kubuni miradi itakayowanufaisha wananchi wa Serengeti. Katibu
Tawala amewataka watumishi wa umma kujiendeleza kielimu na kuongeza maarifa ili
kuongeza ufanisi wa kazi wakiwa kazini “Msibweteke na elimu mlizonazo na
kusahau kwenda kujiendeleza kielimu” alisema Mapunda. Aidha Mapunda
amewataka watumishi wa umma kutumia vizuri kipato wanachopata kwa kujiwekea
akiba na kufanya shughuli za maendeleo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mhe. Juma Porini Keya
ambaye pia alihudhuria kikao hicho amempongeza Bw. Mapunda kwa uteuzi na
kuahidi kutoa ushirikiano katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Serengeti na
kuwataka watumishi wa Halmashauri kuyafanyia kazi yale yote aliyosema Katibu
Tawala Mkoa wa Mara.
Tarehe 10 Septemba 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John
Pombe Magufuli alimteua Bw. Ado Stephen Mapunda kuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mara
na kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Benedict Ole Kuyan ambaye amestaafu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mara (kushoto) Bw. Ado Stephen Mapunda Akiwasili katika
Ukumbi wa Mikutano wa Halamshauri, kulia ni Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti
Bw. Cosmas Qamara
akimkaribisha Katibu Tawala Mkoa wa Mara tayari kwa mazungumzo na watumishi.
Sehemu ya watumishi waliojitokeza kumsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Mara
No comments:
Post a Comment