Monday, 26 September 2016

NAIBU WAZIRI WA OR-TAMISEMI AFANYA ZIARA WILAYANI SERENGETI

Habari toka Kitengo cha Habari na Mawasiliano, HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI

Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI (Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) Suleiman Saidi Jafo, leo tarehe 26 Septemba 2016 amefanya ziara katika Wilaya ya Serengeti na kufanya kikao na watumishi wa Serikali kutoka taasisi mbali mbali, viongozi wa kisiasa pamoja Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu.

Katika kikao hicho Waziri Jafo amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu katika kuibua miradi itakayowanufaisha wananchi wote Wilayani Serengeti. Pia amewataka watumishi wote wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuepuka vitendo vya rushwa na kukwamishwa shughuli za maendeleo. 

Aidha Waziri Jafo amefanya ukaguzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 3 inayojengwa na Mkandarasi Samota Construction katika Mji wa Mugumu na kuridhishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia. Katika ukaguzi huo Waziri Jafo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilika haraka na kuzingatia ubora wa kazi. 

Waziri Jafo pia amefanya ukaguzi katika majengo ya hospitali ya Wilaya ambayo ujenzi wake bado haujakamilika.  Katika ukaguzi huo Waziri Jafo ameahidi kulichukua suala hilo la kukwama kwa ujenzi huo na kulifikisha katika ngazi husika. Akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Jafo alisema “Hospitali hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Serengeti na pia watalii wanaofika katika Hifadhi ya Serengeti wanaweza pata huduma hapa pindi wanapougua”

Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Serengeti umekwama kutokana na ukosefu wa fedha ambapo mpaka sasa huduma za matibabu ya ngazi ya Wilaya zinatolewa katika Hospitali ya Nyerere (NDDH) inayomilikiwa na kanisa la Menonite Tanzania.

                                        MATUKIO KATIKA PICHA
    Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI (wa pili upande wa kulia) akiwasili katika ukumbi wa mkutano
    katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.  Katikati ni Mbunge wa Jimbo
    la Serengeti Marwa  Ryoba, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu.


    Mhandisi wa Ujenzi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Sospeter Leonidas akifafanua jambo
    kuhusu ujenzi wa barabara ya lami katikaMji wa Mugumu kwa     Naibu Waziri wa
    OR-  TAMISEMI, Suleiman Jafo




No comments:

Post a Comment