Wednesday, 28 September 2016

DC SERENGETI AIPONGEZA PSPF KWA KUTOA HUDUMA NZURI

Habari toka kitengo cha Habari na Mawasiliano HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI.


Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu ameipongeza Taasisi ya Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa umma kwa huduma nzuri wanazotoa kwa wateja wao.
Pongezi hizo zimetolewa katika semina iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ambapo wataalamu kutoka PSPF walikutana na watumishi wa serikali kutoka taasisi mbali mbali ndani ya wilaya ya Serengeti.

Katika hotuba aliyotoa, Babu alisema “Taasisi ya PSPF imekuwa na mchango mkubwa kwa serikali katika kuwahudumua watumishi wa serikali kwa kutunza amana zao pamoja na kutoa mikopo inayowanufaisha wateja wake nawapongeza sana kwa huduma zenu nzuri mnazotoa” aliendelea kwa kusema “watumishi tumieni fursa zitolewazo na PSPF katika kufanya shughuli za kimaendeleo”
Akiongea kuhusu huduma wanazotoa, Meneja wa PSPF Mkoa wa Mara, Bwana Deogratius Njuu alisema “PSPF tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa tunatoa huduma bora kwa wateja wetu” aliongezea kwa kusema kuwa “Wateja wa PSPF wananufaika na mkopo wa kujikimu unaotolewa kwa watumishi wapya, mkopo wa kujiendeleza kielimu na pia tunatoa mikopo ya viwanja vilivyopimwa kwa ajili ya makazi”
Aidha watumishi walioudhiria semina hiyo waliipongeza PSPF kwa kuwafikia katika maeneo ya kazi na kuwaomba kuboresha mahusiano zaidi na wateja wao na kufika vijijini pia kutoa elimu hiyo. 

                                          MATUKIO KATIKA PICHA
Meneja wa PSPF Mkoa wa Mara Bw. Deogratius Njuu akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu
















Monday, 26 September 2016

NAIBU WAZIRI WA OR-TAMISEMI AFANYA ZIARA WILAYANI SERENGETI

Habari toka Kitengo cha Habari na Mawasiliano, HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI

Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI (Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) Suleiman Saidi Jafo, leo tarehe 26 Septemba 2016 amefanya ziara katika Wilaya ya Serengeti na kufanya kikao na watumishi wa Serikali kutoka taasisi mbali mbali, viongozi wa kisiasa pamoja Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu.

Katika kikao hicho Waziri Jafo amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii na kuwa wabunifu katika kuibua miradi itakayowanufaisha wananchi wote Wilayani Serengeti. Pia amewataka watumishi wote wa Serikali kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuepuka vitendo vya rushwa na kukwamishwa shughuli za maendeleo. 

Aidha Waziri Jafo amefanya ukaguzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilometa 3 inayojengwa na Mkandarasi Samota Construction katika Mji wa Mugumu na kuridhishwa na hatua ya ujenzi ilipofikia. Katika ukaguzi huo Waziri Jafo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Juma Hamsini kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unakamilika haraka na kuzingatia ubora wa kazi. 

Waziri Jafo pia amefanya ukaguzi katika majengo ya hospitali ya Wilaya ambayo ujenzi wake bado haujakamilika.  Katika ukaguzi huo Waziri Jafo ameahidi kulichukua suala hilo la kukwama kwa ujenzi huo na kulifikisha katika ngazi husika. Akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Jafo alisema “Hospitali hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Serengeti na pia watalii wanaofika katika Hifadhi ya Serengeti wanaweza pata huduma hapa pindi wanapougua”

Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Serengeti umekwama kutokana na ukosefu wa fedha ambapo mpaka sasa huduma za matibabu ya ngazi ya Wilaya zinatolewa katika Hospitali ya Nyerere (NDDH) inayomilikiwa na kanisa la Menonite Tanzania.

                                        MATUKIO KATIKA PICHA
    Naibu Waziri wa OR-TAMISEMI (wa pili upande wa kulia) akiwasili katika ukumbi wa mkutano
    katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.  Katikati ni Mbunge wa Jimbo
    la Serengeti Marwa  Ryoba, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Nurdin Babu.


    Mhandisi wa Ujenzi Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Sospeter Leonidas akifafanua jambo
    kuhusu ujenzi wa barabara ya lami katikaMji wa Mugumu kwa     Naibu Waziri wa
    OR-  TAMISEMI, Suleiman Jafo




Sunday, 18 September 2016

VIJIJI 33 SERENGETI KUNUFAIKA NA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI

Habari toka Kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikishirikiana na wadau wake Shirika la Hifadhi ya Serengeti (SENAPA) pamoja na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) imeanza kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya Vijiji vya Wilaya ya Serengeti kupitia ufadhili wa Benki ya Wananchi ya Ujerumani (KfW).
“Mpango wa matumizi bora ya ardhi ni endelevu na muhimu kwa kizazi cha sasa na baadae” alisema Dk. Malogo Kongola ambae ni Mshauri elekezi wa Mradi kutoka FZS katika mkutano wa kutambulisha mradi kwa serikali ya Kijiji cha Singisi kilichopo Kata ya Nagusi.
Akitoa shukrani zake za dhati kwa wahisani kuwezesha kijiji chake kuwa miongoni mwa vijiji vilivyopata mradi huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Singisi Bw. Giroida Dabdera alisema “Mpango huo utawasaidia wakazi wa kijiji chake kupanga na kutumia vizuri rasilimali zilipo kijijini na kuondoa migogoro iliyopo kati ya wakulima, wafugaji na wadau wengine watumia ardhi” Naye Diwani wa Kata ya Nagusi Mhandisi Dickson Manyeresa ameiasa Serikali ya Kijiji kuhakikisha wanabainisha maeneo yote muhimu kwenye mpango na kutenga matumizi kulingana na mahitaji ya sasa na baadae.
Mpango huo umekuja wakati mwafaka ambapo Rais John Pombe Magufuli akiwa tayari ameiagiza Tume ya Taifa ya Mipango na Matumizi ya Ardhi (NLUPC) kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020, jumla ya vijiji 7,500 viwe na mpango endelevu wa matumizi bora ya ardhi.
Wilaya ya Serengeti ina jumla ya Vijiji 78 ambapo mpaka sasa ni vijiji vitano pekee vilivyokuwa na mpango endelevu wa matumizi bora ya ardhi, huku vijiji 33 vikitarajiwa kunufaika na ufadhili huo. 

                          MATUKIO KATIKA PICHA






Wednesday, 7 September 2016

ZIARA YA MKUU WA MKOA WA MARA WILAYANI SERENGETI


Habari toka kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

 Mkuu wa wilaya ya Serengeti Nurdin Babu (Kulia) akimpokea Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa




Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa jana tarehe 06 Septemba 2016 amefanya ziara ya kujitambulisha katika Wilaya ya Serengeti na kukutana na watumishi wa taasisi za serikali, taasisi zisizo la serikali, viongozi wa dini, wadau wa maendeleo pamoja na waheshimiwa madiwani.



Katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu aliwasilisha kero kubwa mbili zinazowakabili wananchi ambazo ni Ukosefu wa Maji Safi na Salama pamoja na Uharibifu wa Mali na Mazao unaofanywa na Tembo wanaovamia vijiji hata kufikia hatua ya kuuwa wananchi.



Dk. Mlingwa akijibu, alisema kuwa “Anazitambua kero hizo na juhudi za dhati zinafanyika kutatua kero hizo kwa wananchi wa wilaya ya Serengeti” Kuhusu ukosefu wa maji safi na salama katika mji wa mugumu alisema kuwa, “ Ni mwezi wa nne (4) sasa wakazi wa mugumu hawana maji na kuiagiza idara husika kuhakikisha maji yapatikana mapema iwezekanavyo” Dk. Mlingwa ametilia mkazo suala la maendeleo na kuzitaka taasisi husika ndani ya wilaya ya Serengeti kusukuma gurudumu la maendeleo ili kuleta tija kwa Wilaya na Mkoa wa Mara kwa ujumla.



Aidha Dk. Mlingwa ameipongeza Halmshauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuhakikisha mji wa mugumu unapata lami huku Mkandarasi SAMOTA Construction Ltd akiwa yupo eneo la kazi akiendelea na hatua za awali ya uwekaji wa lami. Hata hivyo Dk. Mlingwa amesikitishwa na uchelewaji wa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Butiama mpaka Mugumu Serengeti huku akitilia mashaka uwezo wa wakandarasi hao kukamilisha awamu hiyo ya kwanza ya barabara ya lami ya kilometa 50 itakayoishia Sanzati.


Dk. Mlingwa alipata muda wa kutembelea Bwawa la Machira na kuona jitihada za Halmashauri pamoja na Idara ya maji Mji wa Mugumu kurejesha hali ya upatikanaji wa maji. Ziara hiyo ya siku 3 pia itahusisha kutembelea miradi ya afya na maji ndani ya Wilaya ya Serengeti.



                        MATUKIO KATIKA PICHA
















Sunday, 4 September 2016

HARAMBEE YA UKAMILISHAJI UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI ROBANDA TAREHE 2 SEPTEMBA 2016



Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu (kushoto) akisalimiana na Mgeni Rasmi wa Harambee hiyo Mhifadhi Mkuu Hifadhi ya Taifa ya Serengeti Bw. William Mwakilema.

Harambee ya ukamilishaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Robanda iliyofanyika katika majengo ya shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Robanda imefanikiwa kupata jumla ya fedha taslimu Tsh Milioni 11,299,000 na fedha za kigeni 13 US Dollars zilipatikana papo hapo pamoja na ahadi ya fedha kiasi cha Tshs Mil 42,499,500 fedha za kigeni 2,000 US Dollars, Mifugo Ng'ombe watano (5), mbuzi wawili (2). Serikali ya kijiji cha Robanda imeahidi kujenga nyumba moja (1) ya kuishi walimu huku Kampuni ya Thomson Safari ikiahidi kujenga nyumba tatu za kuishi walimu na kuwa na jumla ya nyumba nne (4) zote zikiwa na thamani ya Tshs Milioni 290. Mifuko ya Saruji 237 iliahidiwa kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kutoka kwa wadau mbali mbali wa maendeleo walioshiriki harambe hiyo. Aidha Benki ya Posta tawi la Musoma imechangia madawati 50, huku wadau wengine wa maendeleo kuongezea madawati manne (4) na kufanya idadi ya madawati yaliyochangiwa kufikia 54. Akitoa shukrani za dhati Mgeni rasmi katika harambee hiyo Mhifadhi Mkuu toka HIfadhi ya Taifa ya Mbuga ya Wanyama Serengeti Bw William Mwakilema alisema “anashukuru wale wote walioguswa na kuchangia ujenzi wa shule hiyo kwani kukamilika kwake kutasaidia wanafunzi waishio maeneo jirani na robanda kuwa na shule karibu na kuondoa adha ya umbali mrefu wanaotumia wanafunzi hao kwenda shuleni”
Harambe hiyo iliudhuliwa na Mkuu wa Wilaya ya serengeti Mhe. Nurdin Babu, Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Bw. Cosmas Quamara na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini Seph pamoja na Waheshimiwa Madiwani pia walijitokeza kuunga mkono Mhe. Diwani wa Kata ya Ikoma Mhe. Michael Kunani huku wageni kutoka ndani na nje ya wilaya ya serengeti walijitokeza na kufanikisha upatikanaji wa michango hiyo. Mpaka sasa shule hiyo bado haijaanza kupokea wanafunzi kutokana kutokamilika kwa baadhi ya majengo zikiwemo nyumba za walimu. kukamilika kwa majengo na uwekaji wa thamani kutaboshera hali ya elimu katika kata ya Ikoma.

                            MATUKIO KATIKA PICHA 
Mhe Diwani Kata ya Ikoma Bw. Michael Kunani (kushoto) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya Serengeti Mhe. Nurdin Babu (kati kati) kushoto ni Afisa Tarafa wa Grumet Bw, Paul Shanyangi
Mhe Diwani Kata ya Ikoma (kushoto) akimkaribisha Mgeni Rasmi wa Harambee (kulia) Mhifadhi Mkuu SENAPA Bw. William Mwakilema


Wadau wa maendeleo walijitokeza kwa wingi na kuchangia maendeleo kata ya Ikoma




Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Bw. Juma Hamsini Seph

Katibu Tawala Wilaya ya Serengeti Bw. Cosmas Quamara

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti/ Diwani wa Kata ya Natta Mhe. Juma Porini Keya


Jumla ya Tsh Mil 11,299,000  zilichangwa papo hapo.