Wednesday, 30 November 2016

KIJIJI CHA NYAMISINGISI WILAYANI SERENGETI KUANDAA NA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI.

Habari toka Kitengo cha TEHAMA & UHUSIANO
HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI.

Kijiji cha Nyamisingisi kilichopo Kata ya Issenye Wilayani Serengeti katika Mkoa wa Mara kunufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi.


 Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ikishirikiana na wadau wake wa maendeleo; Shirika la Hifadhi ya Serengeti (SENAPA) pamoja na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) kupitia ufadhili wa Benki ya Wananchi wa Ujerumani(KfW) wamejikita katika kuhakikisha vijiji vilivyo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti pamoja na pori la akiba la Grumeti na Ikorongo kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi.  “Tunashukuru kwa kupata fursa hii, mpango huu ni mojawapo ya kipaumbele kikuu katika kijiji hiki” alisema Diwani wa Kata ya Issenye Mhe. Mosi Nyarobi alipokuwa akiwakaribisha wajumbe wa timu ya matumizi bora ya ardhi ya Wilaya ya Serengeti katika kikao kilichofanyika na Serikali ya kijiji hicho leo tarehe 30 Novemba 2016.

Aidha wanakijiji kwa kauli moja kupitia mkutano maalum wa Kijiji uliofanyika siku hiyo hiyo wameridhia kuundwa kwa kamati ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji yenye wajumbe nane. Kamati hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Kijiji kwa pamoja itaandaa rasimu ya mpango wa matumizi bora ya ardhi ya Kijiji cha Nyamisingisi.









No comments:

Post a Comment