Sunday, 28 August 2016

DC NURDIN BABU KUPAMBANA NA MAFATAKI WALIOWAKATISHA MASOMO WANAFUNZI 42

Habari na Anthony Mayunga. (www.mwananchi.co.tz)

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu

Serikali wilayani Serengeti, Mkoa wa Mara imeapa kupambana na
wanaume waliowakatishia masomo wanafunzi wa kike zaidi ya 42 wa shule za msingi na sekondari kwa kuwapa ujauzito. Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu katika mkutano wake na wakazi wa mji wa Mugumu alimwagiza kamanda wa polisi wilayani humo kuwakamata wanaume wanaodaiwa kuwapa ujauzito wanafunzi hao na kuwafikisha mahakamani. Pia, aliagiza wazazi wa wanafunzi hao ambao wanawalinda waliowapa ujauzito wakamatwe na kufikishwa mahakamani. “OCD kamata wazazi na watoto ambao watajaribu kuficha ukweli na wafikishwe mahakamani kwa kuwa kumeibuka mtindo wa wazazi kushirikiana na watoto na anapoulizwa aliyempa mimba hamjui, wenye majibu kama hayo kamata wote,” alisema Babu.

Friday, 26 August 2016

VIKUNDI VYA WATOTO WAISHIO MAZINGIRA HATARISHI WILAYANI SERENGETI VYANUFAIKA NA MIKOPO.

Habari na Serengeti Media Centre
(www.serengetimediacentre.blogspot.com)

Zaidi ya Tsh Milioni 308 zimekopeshwa kwa vikundi 96 vya Watoto waishio katika Mazingira Hatarishi kupitia Mradi wa Pamoja Tuwalee wilayani Serengeti Mkoa wa Mara kwa kipindi cha mwaka 2011 hadi 2016.
Mradi wa Pamoja Tuwalee ambao umefikia ukomo ulikuwa unaendeshwa na Shirika la Pact Tanzania kwa kushirikiana na asasi ya BAK-AIDS kwa ufadhili wa USAID/PEPFAR katika kata 17 kati ya 30 za wilayani hapa,na kuwezesha akina mama wengi kujihusisha na shughuli za bustani za mboga mboga ambazo zimewawezesha kuweka akiba.
Mratibu wa Mradi wa BAK-AID wilaya ya Serengeti Christopher Genya kwenye kikao cha wadau wa maendeleo wilaya wakati wa kukabidhi shughuli za mradi huo kwa  halmashauri alisema,vikundi hivyo vina akiba y ash 331,162,260,na wanaendesha biashara mbalimbali 1473 katika maeneo yao.
“Kupitia mradi huu watoto 4517 kati ya 8,046 wanalelewa na walezi walio katika vikundi,na kaya 1,839 zimenufaika na mradi huo na wameweza kuboresha makazi yao,wengine wamenunua mifugo,na waliokuwa wanakula mlo mmoja sasa wanakula milo mitatu,na mafanikio makubwa ni kwamba wanajisimamia wenyewe,”alisema.
Hata hivyo alisema katika utekelezaji wa mradi huo walikabiliana na changamoto za baadhi ya kamati za watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi kutokuwasaidia watoto,ikiwemo kutokushirikishwa katika vikao vya serikali za vijiji na kata.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ambaye pia ni afisa maendeleo ya jamii Sunday Wambura aliwataka wadau wa maendeleo kuhakikisha katika shughuli zao wanaweka mipango ya kuwasaidia watoto wa mazingira hatarishi,kwa kuwa hilo ni jukumu la kila mmoja.
Mapema afisa mradi huo Eza Yusuph alisema lengo kuu lilikuwa kuimarisha mifumo iliyopo ya jamii na familia zao,kuongeza rasilimali za ndani na nje katika kufikia mahitaji ya watoto na  mfumo wa ustawi wa familia baada ya kukosekana kwa msaada toka nje.


                                                         MATUKIO KATIKA PICHA

Mratibu wa mradi wa pamoja Tuwalee wilaya ya Serengeti Christopher Genya kulia akimkabidhi nyaraka za mradi huo ambao umemaliza muda wake Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya Sunday Wambura katikati ni Afisa Ustawi wa Jamii Faustine Matesi.




Wadau katika picha ya Pamoja.

WALIMU SERENGETI KUTUMIA VISHIKWAMBI (TABLET) KUTUMA TAARIFA TAMISEMI

Habari na Englibert Kayombo
 
Walimu wakuu 109 kutoka shule za msingi Wilayani Serengeti wamewezeshwa mafunzo ya utumiaji wa mfumo wa taarifa za shule (School Information System - S.I.S) kwa kutumia vishikwambi (Tablet)
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofadhiliwa kupitia programu ya EQUIP Tanzania yalianza tarehe 25 Agosti na kukamilika 26 Agosti 2016 katika shule ya Msingi Kambarage iliyopo katika Mji wa Mugumu yamewawezesha walimu hao pia kupatiwa kishikwambi kwa kila mmoja.
Akiongea kuhusu mafunzo hayo, Mwezeshaji kitaifa wa Mfumo wa School Information System Bw. Victor Mkama alisema "Mafunzo hayo ni muhimu kwa walimu ili kuweza kutumia vishikwambi hivyo bila matatizo na kuwajengea uelewa wa umuhimu wa kutuma taarifa kwa kutumia njia ya mtandao" Mwezeshaji aliendelea kwa kusema kuwa "wametoa vishikwambi 109 kwa walimu wakuu wote wa shule za msingi wilayani serengeti vyenye thamani ya Milioni 38.1 ili kuweza kutuma taarifa muhimu zinazohusu shule waliyopo moja kwa moja TAMISEMI" Vishikwambi hivyo vitatumika katika ukusanyaji wa taarifa muhimu zikiwemo idadi ya walimu, wanafunzi, madarasa, madawati, matundu ya vyoo pamoja na nyumba za walimu na rasilimali zinazopatina katika maeneo ya shule na kutumwa moja kwa moja TAMISEMI hivyo kupunguza usumbufu wa upatikanaji wa taarifa uliokuwa ukiipata Serikali.








MWENGE WA UHURU WILAYANI SERENGETI TAREHE 20 AGOSTI 2016

Mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Mara zimehitimishwa Jumapili ya tarehe 21/08/2016 baada ya kuzunguka wilaya zote sita za mkoa wa mara na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo. Mwenge wa Uhuru uliingia Wilayani Serengeti siku ya Jumamosi ya tarehe 20/08/2016 kupitia Kata ya Nyansurura, aidha mwenge huo ulizunguka wilayani na kuzindua miradi sita maendeleo yenye thamani ya jumla ya Tshs Milioni 755,437,611.00 na hatimae kukabidhiwa siku ya jumapili ya tarehe 21/8/2015 Mkoa wa Arusha.    

Kauli Mbiu ya Mbio za Mwenge kwa Mwaka huu inasema kuwa VIJANA NI NGUVU KAZI YA TAIFA WASHIRIKISHWE NA KUWEZESHWA.
Viongozi mbali mbali kutoka Wilaya ya Serengeti tayari kuupokea Mwenge wa Uhuru


Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu (Kulia) akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Tarime Mhe. Glorious Luoga.


Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa (kushoto) akiwasili katika kijiji cha Oloisakwaine kilichopo wilaya ya loliondo tayari kumkabidhi Mwenge wa Uhuru Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo.


Mkimbiza Mwenge Kitaifa Ndg. George Jackson Mbijima Akiingia katika Wilaya ya Loliondo, Mkoa wa Arusha.






Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mhe. Nurdin Babu (kushoto) Mwenge wa uhuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa tayari kuupeleka Mkoa wa Arusha.








Mwenyekiki wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhe. Juma Porini Keya








Msafara wa Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Serengeti kuelekea Wilaya ya Loliondo Mkoa wa Arusha.